Nyakati Tatu Muhimu Za Kufanya Ibada – Zisikupite Katika Ramadhaan


1-Wakati wa mwanzo: Baina ya Alfajiri na jua kuchomoza:

Usimulizi uliothibiti kutoka katika Swahiyh Muslim (564/1) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba walikuwa wakibakia macho wakati huo hadi jua kuchomoza kwani ni wakati mja anapogaiwa rizki yake, na ni wakati wenye kheri nyingi, unampa siha nzuri ya mwili binaadamu, na kwa ujumla ni wakati wenye baraka nyingi za kila aina kwani Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba:

((Ewe Allaah, wabarikie Ummah wangu nyakati za asubuhi mapema)) [At-Tirmidhiy, Ahmad, Abu Daawuud, Ibn Maajah na imethibitishwa kuwa ni Hadiyth Swahiyh na Shaykh Al-Albaaniy]

2- Wakati wa pili: Kabla ya Jua kuzama (Magharibi):Huu ni wakati ambao bado Muislamu yuko katika Swawm na du'aa yake anayoiomba hairudi:

Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (([Watu] watatu du'aa zao hazirudi; mwenye kufunga hadi afuturu/afutari, Kiongozi muadilifu na aliyedhulumiwa)) [At-Tirmidhiy kwa isnaad nzuri]

Kwa hiyo ni fursa ya kuitumia Muislamu aombe du'aa na haja zake wakati huu khaswa pia kwa vile ni wakati ambao Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amehimiza Atukuzwe kama Anavyosema:

((.. na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa)) [Qaaf: 39]

((…Na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumsifu kabla ya kuchomoza jua, na kabla halijachwa, na nyakati za usiku pia umtakase, na ncha za mchana ili upate ya kukuridhisha)) [Twaahaa: 130].

((…Na omba msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi jioni na asubuhi)) [Ghaafir: 55]((…Na omba msamaha kwa dhambi zako, na umtakase Mola wako Mlezi kwa kumhimidi jioni na asubuhi)) [Ghaafir: 55]3- Wakati wa tatu: Suhuur - Kabla ya AlfajiriAllaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amewaaahidi Wacha Mungu Pepo kwa sababu sifa mojawapo yao ni kuomba maghfira kabla ya Alfajiri:

((Hakika Wacha Mungu watakuwa katika Mabustani na chemchem)) ((Wanapokea Aliyowapa Mola wao Mlezi. Kwa hakika hao walikuwa kabla ya haya wakifanya mema)) ((Walikuwa wakilala kidogo tu usiku)) ((Na kabla ya Alfajiri wakiomba maghfira)) [Adh-Dhaariyaat: 15-18]

Kisha wamesifiwa tena kwa sifa hiyo hiyo pamoja na nyinginezo:
((Wanaosubiri, wanaosema kweli, na watiifu, na wanaotoa sadaka, na wanaoomba maghafira kabla ya Alfajiri)) [Al-'Imraan: 17]

Muislamu asiache wakati huo umpite kwani ni wakati muhimu na wenye fadhila na faida kubwa kwa vile Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka wakati huo kutoka mbingu ya saba na kuweko mbingu ya ardhi kutukidhia haja zetu:

Imetoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) kwamba Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: (Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia (mbingu ya kwanza) inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba Nimtakabalie? Nani ana shida Nimtekelezee? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Nani miongoni mwetu asiyemhitaji Mola wake kumkidhia haja zake na kumuondeshea shida zake? Nani asiyekuwa na madhambi asiyemhitaji Mola wake kumghufuria? Hivyo usiache wakati huu ukakupita khaswa kwa vile mwezi huu Mtukufu ambao kila jambo ulifanyalo lina fadhila na thawabu marudufu.Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atuwezeshe kudiriki nyakati hizo tatu na nyingine, tuwe katika ibada katika mwezi huu wa Ramadhaan na miezi yote mingineyo na Atujaalie kheri na Baraka nyingi, Atukidhie haja zetu, Atuondoshee shida zetu na Atughufurie madhambi yetu yote. Aamiyn.

Kwa mawaidha zaidi alhidaaya
 Mashughuli

Phasellus facilisis convallis metus, ut imperdiet augue auctor nec. Duis at velit id augue lobortis porta. Sed varius, enim accumsan aliquam tincidunt, tortor urna vulputate quam, eget finibus urna est in augue.

No comments:

Post a Comment